Fainali Uzeeni? 

Mtazamo tofauti kuhusu Uzee.

Kwani uzee ni nini mpaka iwe kitu cha kuhuzunisha? Uzee umeakua kama tusi, neno hili linatumika kumuonesha muhusika kuwa amechakaa, amefuja, amepoteza nuru. Uzee umekua kama laana au ulemavu. 

Leo nikiwa naelekea mjini, nilipanda daladala nikakutana na mama mwenye umri mkubwa kidogo, anaweza kuwa na miaka 60 au zaidi. Alikua amevaa gauni la kitenge lililomshika mwili kidogo, refu mpaka chini, rangi ya njano. Kiunoni alijifunga na mkanda wa ngozi ulionakshiwa na shanga za rangi mbalimbali, kichwani akiwa amejipamba na  kilemba, uso wake ulikua unateleza , alikua amejipaka mafuta mengi. Akaniuliza swali, kitu gani kinakufurahisha? Nikasita kujibu, nikamuuliza tena kwa mshangao, ‘ kitu gani kinanifurahisha?’ . Akajibu ‘ndio.’ Na huo ulikua mwanzo wa mazungumzo na bibi huyu. Nikagundua kuwa watu wanaweza kuzeekaa, lakini nafsi zao hazieeki. Miguu yao inaweza isiwe na nguvu, macho yao yanaweza yasione vizuri lakini nafsi zao zimejaa hekima, ndoto, furaha, na hata nguvu. Wazee ni vijana walioishi muda mrefu. Nmegundua uzee sio mwisho wa maisha. Unaweza ukawa kijana na maisha yako yakawa mafupi. 

Kwanini tuelekee uzee kama vile ndio mwisho wetu? Wakati kifo kinaweza tokea wakati wowote? 

Jamii yetu inatangaza ujana, inapenda ujana, inaabudu ujana. Ujana sio kitu kibaya, fahamu kuwa ujana ni hatua kama ilivyo utoto, kuna wakati utafika tutavuka hatua hiyo. Ni wazi kwamba ujana ni wakati binadamu anakua na nguvu zaidi, hivyo anaweza kufanya mambo makubwa zaidi. Hata hivyo ujana sio jambo la umilele, ujana hupita. 

Jamii yetu imezungukwa na vijana, asilimia 60 ya watu Tanzania ni vijana , takwimu zinaonesha kufikia mwaka 2040 asilimia 40 ya vijana duniani watakua ni waafrika. Usifurahie sana, maana wakati huo unaweza usiwe kijana tena, ila furahia utakua katika hatua nyingene ya ukuaji wa binadamu. Kama kijana ni muhimu kutumia muda wako na nguvu zako vizuri.

Uzee ni tija, uzee ni sifa, uzee ni baraka , inamaana umeona mengi na pengine unajua mengi. Dr. Deo Lubala hupenda kusema ukiwa kijana na utabia mbaya, ukizeeka unazeeka na tabia yako. Hivyo mbali na baraka ya kuishi miaka mingi, unaweza ukawa mzee na ni mjinga, mzembe, mchafu, mwizi nk. Utamaduni wetu umetufundisha kuheshimu watu waliotuzidi umri, yaani wazee. Tuwape heshima zao, lakini wewe kama mzee mtarajiwa, usikubali kuzeeka na tabia mbaya.