Uongo Uliojificha Nyuma Ya Fikra “Waifu Matirio”
Mtazamo wa ‘waifu matirio’ na namna unavyowakandamiza wanawake.
Hivi hili jambo hata lina ukweli? Mimi ni mke lakini mpaka leo najiuliza kama na mimi ni “waifu matirio”.
Huu ni mtazamo maarufu katika mitaa ya jamii za Kiafrika, ni wazo linalomaanisha kuwa kuna yule mwanamke ambaye ana vigezo vya kuwa mke. Inasemekana vigezo hivi ni kama kuitunza nyumba, na kumpikia mume, yaani inazungumzia lile jukumu la kiutamaduni la mwanamke katika nyumba. Ni lazima niseme kuwa sioni kusudi katika majukumu hayo kwasababu ninajua mimi ni zaidi ya kuwa mke. Sikuzaliwa ili tu kuwa kitu kimoja, mke.
Swali ni kwamba kwanini hakuna anayezungumza kuhusu “hazbendi matirio”? Ninaamini Hakuna “waifu matirio” wala “hazbendi matirio”. Bali kuna watu wazima waliopevuka kifikra.
Mabinti wengi wanafundishwa tokea wakiwa na umri mdogo jinsi ya kuwa wake bora, mabinti hawa wanajikuta tu wanakua na kuwa waangalizi, na kuwa duni kwa wanaume, katika baadhi ya familia baina ya ndugu na ndugu, wavulana hupokea vitu vingi vizuri kuliko wasichana, na wavulana watapewa fursa za kukutana na wenzao, msichana atabaki ndani kwa ajili ya kuosha vyombo, anaandaliwa kuwa mke. Je! Ulijua kuwa takribani wasichana na wanawake milioni 130 ndani ya Afrika waliolewa katika utoto?
Kulingana na ripoti ya ndoa za utotoni Afrika iliyoandaliwa na Kituo cha Haki za Binadamu mwaka 2018, inakadiriwa kuwa angalau asilimia 55 ya wasichana huko nchini Mali wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18, na asilimia 15 wanaolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 15.
Picha imeandaliwa na Dazzle Jam katika Pexels.com
Hii inathibitisha namna ambavyo mtoto wa kike anachukuliwa, katika umri mdogo kabisa anaonekana kama mke mtarajiwa. Tatizo pekee la suala hili ni kwamba, hii ndio tafsiri pekee anayopewa, kitu pekee anachokumbushwa kila siku. Je! Mwanamke hayuko zaidi ya hapo? Zaidi ya kuwa mke? Baadhi ya tamaduni hata huamua kubana matumizi na kuamua kuikomesha elimu yake eti kwasababu tu ataolewa. Wanawake wengine pia, hawajitumi wakitegemea kuolewa kutawatoa kimaisha.
Wanawake hutazamiwa kuwa wake kiasi kwamba hata katika wakati wa kutongozana baadhi ya wanaume hujifanya kana kwamba wanammiliki mwanamke husika na kuendesha shughuli zake, fedha zake n.k. Huko mtaani wanaume wasiojua chochote kuhusiana na yeye watazungumza kama vile wana mamlaka juu yake. Rafiki yangu mmoja Mhindi huwa hafuniki nywele zake ama kuvaa kitamaduni ila inatokea mpita njia anakosoa uvaaji wake. Kwanini hatusikii udhalilishaji huo wakielekezewa wanaume? Kuna matarajio kwamba mwanawake hatakiwa kuenenda na kujiweka kwa namna fulani kwasababu anahitaji kuonekana anafaa kwa ndoa.
Kulingana na namna walivyolelewa wasichana, ndoa inatazamwa kama tuzo kwa mabinti wengi, baadhi huiita bahati, lakini ndoa ni uamuzi tu, ndoa si harusi hivyo hakikisha shangwe yako haiishii hapo. Baadhi ya wanaume, hudhani kuwa wanampa mwanamke msaada kwa kumuoa, na baadhi hufikiri kwamba wanaificha aibu yake, huu ni upotofu kwasababu ndoa ni haki ya kisheria ya wote mwanaume na mwanamke.
Picha imeandaliwa na Plavalaguna katika Pexels.com
Pale mwanamke anapofikia katika miaka yake ya 30 na, alafu akawa hajaolewa, watu wataanza kujadili ana tatizo gani. Je! Kunaweza kuwa na tatizo gani katika wewe kuwa mwenyewe? Baadhi ya wanawake hukosa kujiamini na kupatwa na sonona kwasababu wanafikiri wamechelewa, hawana mvuto, au hawana bahati, ni kwanini kuwa mke iwe ndio kipimo cha mafanikio kwa mwanamke? Je! Wanawake hawana hamasa zingine maishani? Kuna shinikizo sana katika kuolewa lakini haijaandikwa popote katika katiba ya nchi yetu.Ndoa hutafsiriwa chini ya Sheria ya ndoa ya Tanzania Kifungu s.9 kama ‘muunganiko wa ridhaa wa mwanaume na mwanamke uliokusudiwa kudumu katika maisha yao ya pamoja.’ Hakuna aliyechelewa kuingia katika ndoa, ndoa si shahada ambayo kila mmoja anahitaji kuwa nayo. Ni uamuzi, uamuzi wako. Ndoa si tu cheo cha kusherekewa, ndoa ni kuhusiana na majukumu. Kwahiyo, ni muhimu kwa mtu kuelewa majukumu kabla ya kuingia huko, ni vyema mtu awe amekua kimwili na kiakili kabla ya kuingia katika ndoa.
Makala hii imeandikwa na Najma Juma na kutafsiriwa na Chris Masilago
4 thoughts on “Uongo Uliojificha Nyuma Ya Fikra “Waifu Matirio””
Proud of You👊🏾
wawoo yaan hii dhana uliyoiongelea hapa
ipo kabisa kwa asilimia kubwa kwenye jamii yetu ya kiafrika…hapa inabidi Mis Najma hii elimu uliyoiandika hapa nataman kila familia au mashuleni n.k kuwafundisha mabinti kuwa wao hawajazaliwa duniani kwa ajili ya kuwa wife material tu.. watambue kuwa wapo kwa ajili ya vingi kama ilivyo kwa wanaume… yaani uliyoeleza hapo juu ni kweli kabisa jamii yetu ya inaamnyooshea sana Mwanamke kuanzia hata miaka 25 kuwa kwa nini hujaolewa ila mwanaume hata akifikisha miaka 40 haulizwi kitu
Huuu Ni uingo Endeleni kujidanganya
hii dhana ya wife material ni label ya kandamizi ya kisaikolojia