Usiisubiri hatima yako
Wengi tutakuwa tumeusikia usemi huu “hatima yangu mimi ni kuwa mtu mkubwa, kuwa mtu fulani”. Hatima ni mwisho wa mtu fulani. Ni hitimisho au kilele cha mafanikio ya mtu fulani.
Kamusi ya Mirriam Webster inaeleza maana ya neno hatima kama matokeo yasioepukika, matokeo au mwisho wa kitu.
Watu wengi wamekuwa katika hali ya kusubiri hatima zao, kusubiri vilele vya mafanikio yao na wengine hata kutafuta watabiri ili wawape dodoso la ukuu wao katika siku za mbele. Swali ninalojiuliza utafanya nini ukifahamu ukuu wako siku za mbele? Au wakati unasubiri hatima yako unafanya nini? Je mtu akifa leo, hatima yake itakua ipi?
Maswali haya yamenipeleka katika kurasa mbalimbali za mawazo yangu. Inawezekana limekua jambo la kawaida, lakini sio busara kuishi bila kusudi. Mwandishi na msemaji maarufu duniani Myles Munroe aliwahi kusema; “Msiba mkubwa kuliko wote sio kifo bali ni maisha yasiyo na kusudi.” Kama neno lenyewe “kusudi” linavyomaanisha kufanya mambo kwa nia na lengo fulani na sio ilimradi tu, yaani kufanya mambo kimakusudi; Hivyo maisha yetu lazima tuyaishi kimakusudi.
Kwa maana hii, hatima sio mwisho tu bali ni mwisho uliokusudiwa. Hatahivyo, hakuna mwisho bila mwanzo. Hivyo hatima ni matokeo ya kile unachoishi leo. Leo ni mwanzo wa hatima yako. Wengine wanaamini hatima ni maisha waliyochaguliwa kuishi na Muumba au ulimwengu, hivyo hawafanyi lolote bali kusubiria hiyo hatima iwafuate. Ni wazi kama hutochagua kufanya maamuzi ya kuishi hatima yako kila siku utaangukia kuwa mhanga wa tamaduni zinazovuma zenye lengo za kukupotosha na kukandamiza kwa sababu hauna dira ya unapokwenda.
Hatima ipo mikononi mwako kulingana na matendo yako. Unavuna unachopanda. Hatima sio kesho nzuri unayoitamani; bali ni zao la maamuzi na matendo utakayofanya sasa kuifikia kesho hiyo. Mfano: katika nchi kama Tanzania ambayo misingi yake ni ya kidemokrasia, ukipiga kura leo kumchagua mgombea urais, unasababisha mgombea husika kushinda nafasi hiyo. Mgombea huyo anaweza kuwa rais kama atapigiwa kura na watu wengi. Hatima ya kuwa rais ni matokeo ya kura au maamuzi yaliyofanywa mwanzoni kabisa.
Hii ni kanuni inayotumika hata tunavyosomea somo flani ili kuwa mbobezi, hauwezi kuamka asubuhi siku moja na ghafla ukawa mwanasheria au daktari. Unahitaji kuanza mchakato, kila siku kuna kitu unapaswa kukifanya ili kuwa daktari au mwanasheria. Hata aliyekuwa daktari tayari bado anahitaji kufanya kitu kila siku kuendelea kuwa daktari.
Hii inamanisha hatima sio kitu cha kusubiri, bali ni kitu cha kukiishii kila siku. Usiishi ukiisubiri hatima yako. Ishi kuikamilisha hatima yako kila siku. Anza kuishi kimakusudi kwa kuwa na malengo au maono ya mambo unayotaka kufanya kwa ajili ya jamii au familia yako.
5 thoughts on “Usiisubiri hatima yako”
ni kweli kabsaaa, hongera najma kwa ushauri mzuri.
Congratulations Najma
You make me wonder your strength.
You are really very strong.
Such a nice lesson and well written tells who are you. I salute you.
Congratulations.
Thanks alot Peter
Well said Najma
Congrats for this..
Nimejifunza kitu. ‘Kila siku ni fursa ya kufanya jambo la kuboresha au kubadilisha hatima yako.’