Uzushi unaosambazwa juu ya umbo la Mwanamke.
Mtazamo wa jamii kuhusu mwanamke mzuri.
Ni kama vile kitu pekee jamii inachokisherekea kuhusu mwanamke ni umbo na uzuri wake. Katika jamii yetu ya kiafrika kuna maneno kama ‘pisi kali’ na maneno mengine yanayolenga kueleza uzuri wa mwanamke. Hii sio namna ya kumsherekea mwanamke. Wanasherekea mwili wake, wanasifu mapaja yake, midomo na kiuno chake. Je, thamani ya mwanamke katika jamii ni mwili wake tu? Jinsi mwili wa mwanamke ulivyohubiriwa, umesababisha wanawake wengine kutokujiamini kwa sababu hawana hili umbo linalohubiriwa katika jamii, kama kuwa na makalio makubwa, kifua kikubwa ,macho makubwa, umbo namba nane, miguu ya chupa nk. Ni kama vile dunia inajua uzuri wa mwanamke hata kabla hajazaliwa. Mara nyingi umbo la mwanamke linaangaliwa kwa jicho la ngono au hisia za ngono. Noella Thea mtengeneza maudhui maarufu katika mtandao wa Tik Tok alieleza mambo ambayo alitamani mtu angemueleza akiwa katika umri mdogo, alisema “hauhitaji kujiweka katika mwonekano unaochochea ngono ili watu wakupende au kupenda picha zako mtandaoni” .
Propaganda hii ina athari kubwa kwa wasichana wadogo, wale wasio na umbo linalohubiriwa wamekua wakiitwa majina mabaya kama vile ‘kapigwa pasi’ , ‘miguu kama fimbo’ , ‘mtindi mkubwa’ , ‘cheusi’ nk. Kwa sababu hii, wengi wanatafuta kuwa wazuri kama vile uzuri ni bidhaa, wengine wamebadili rangi ya ngozi, kuonesha sehemu za miili yao kupita kiasi , kuchonga maumbo yao au sura ili tu kukubalika au kupendwa zaidi. Kibaya zaidi baadhi ya wasichana wamejenga ujasiri wao juu ya maumbo au shape zao, wameterekeza akili na uwezo wao wa kufikiria na kuchagua kutambulika kwa umbo la miili yao.
Chunguza maudhui ya aina za nyimbo zinazopendwa zaidi, nyingi huzungumzia mwili wa mwanamke. Kwa mujibu wa utafiti huko Marekani, nyimbo zinazohusu hamasa ya ngono zimeongezeka kutoka 18% mwaka 1960 mpaka 41.7% miaka ya 2000. Huku nyimbo zinazohusu mapenzi miaka ya 1960 zilikua ni 70% na kupungua mpka 64% miaka ya 2000. Hii inaonesha namna gani maudhui kuhusu hamasa ya ngono yanavyozidi kukua.
Je, mtoto wa kike anayekua kusikiliza maudhui ya namna hii, na kuona kuwa hana rangi inayokubalika zaidi, au makalio yanayosifiwa zaidi, pua yake na kipimo cha kiuno chake sio cha kimataifa , atakuwa mwanamke wa aina gani? . Propopaganda juu ya mwili wa mwanamke ni kusambaza au kuamini katika fikra kuwa uzuri wa mwanamke ni wa aina moja. Hii sio tu katika maudhui ya mziki, bali hata katika kona za mitaa, hii ni fikra finyu kwani wanawake ni tofauti , hata maumbo yao ni tofauti.
Kusherekea umbo la mwanamke pekee yake, ni kama kusherekea mboga za majani kwa sababu ni za kijani. Thamani ya mboga za majani ipo kwenye virutubisho zaidi na sio kwenye rangi au umbo. Sichukulii poa au kushusha thamani na maajabu ya umbile la mwanamke . Ila siamini kama mwanamke anatakiwa aishi au kuchukuliwa kama ua la mapambo, kila mtu anao uhuru wa kuchagua mwanamke anayemtaka, lakini hana haki ya kuchagua umbo la aina gani linamtambulisha mwanamke.Hata wanaume wanamaumbo, rangi na vimo tofauti. Tunapomuongelea mwanamke, umuhimu wake ndio jambo linalotakiwa kusheherekewa zaidi. Wanawake wamekua nguzo zinazoshikilia familia, wanalea watoto, wengine wamenyimwa haki ya kupata elimu rasmi lakini bado umuhimu wao unaonekana katika kulea familia zao.
Familia ni kitengo kidogo cha jamii na kijito halisi cha utamaduni. Kama kijito hichi kikiwa safi, utamaduni wa watu unamatumaini. Lakini kama kikichafuliwa, yote itakua kama vumbi au majivu maana familia ni msingi wa muundo wa jamii.
― Henry R. Van Til, The Calvinistic Concept of Culture
Kama kitengo kidogo cha jamii, familia inaweza kuwa chombo cha kutengeneza maendeleo ya jamii na taifa. Kama tunataka kulinda kesho ya mtoto wa kike , kama tunataka kuwa na kizazi cha wanawake wanaojiamini, wanaojipenda na kujithamini, kwenye familia ndio mahali pa kuanzia. Kama familia imekua ikituwekea misingi ya maisha tunayoishi , familia inajukumu la kulinda na kueleza ukweli juu ya uzuri wa mwanamke katika ngazi ya kifamilia.
6 thoughts on “Uzushi unaosambazwa juu ya umbo la Mwanamke.”
Mungu akuzidishie Elimu na faham,uzidi kuelimisha maana wasichana wamekosa ufahamu wamepoteza muelekeo,hawajiamini hawatambui thamani yao,kupitia makala hizi mjikite pia kuandaa makongamano na warsha mbalimbali na semina elekezi juu yakuwaelimisha wasichana waliopoteza muelekeo,mtt wakike asitumike km chombo chakumstarehesha muhitaji kwa umbo lake
Asante saaana Auntie wangu. Nitafanyia kazi haya
it’s awesome, It captured the essence of being a woman is not what you see on the exterior, it’s the values, attitudes, knowledge, confidence and so many more, that measure a person and in this article a woman.
this is good, hongera sana. This is very beautiful.
Natamani sana wanawake wa Tanzania wasome haya unayoandika na kutupia katika mtandao wako, naona maelfu ya wake kwa waume wakibadili mitazamo yao na kuwa chanya kila wasomapo makala zako. I’m truly outsmarted, as a man, I must admit. This article like many others of yours, is very insightful.
Asante sana Chris…tuwe mabalozi wa kufikisha ujumbe huu